Mheshimiwa Dkt. Habib Kambanga, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda amekutana na kuzungumza na Bw. Celestine Girukuri ambaye ni mhamasishaji wa matumizi ya Kiswahili nchini Rwanda kwa lengo la kujadili namna ya kuhamasisha matumizi ya Kiswahili nchini humo.  Akizungumza wakati wa majadiliano husika Bw. Girukuri ameufahamisha Ubalozi  kuwa ameandaa andiko dhana linalolenga kuanzisha midahalo itakayofanyika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari na vyuo nchini Rwanda. Lengo la hatua hiyo ni kuwawezesha Wanyarwanda kutumia Kiswahili katika kadamnasi ili kuimarisha uwezo wa kuzungumza Kiswahili pamoja na kukuza umahiri wa kiuongozi.

Girukuri ambaye amewahi kupatiwa mafunzo ya Kiswahili na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ameeleza kuwa kwa kuzingatia kuwa Kiswahili kinazungumzwa zaidi Tanzania ameamua kuanzia Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda na baadaye atazishirikisha taasisi zinazosimamia taaluma.  Kwa upande wake, Balozi Kambanga amemfahamisha kuwa kwa sasa Kiswahili kinakua kwa kasi na ni lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika (AU) na kinatambuliwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu (UNESCO). Hivyo, Balozi Kambanga amesisitiza umuhimu wa Kiswahili kuendelea kuenziwa kwa kuwa ni inatokana na mchanganyiko wa lugha mbalimbali. Sambamba na hilo, Balozi Kambanga amemsitiza Bw. Girukuri kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa Kiswahili ili kuunganisha juhudi.