Mheshimiwa Habib Kambanga, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda ametembelea kampuni ya kuzalisha umeme ya Rusumo  Power Plant Limited  (RPCL) kukagua utekelezaji wa majukumu ya kampuni hiyo inayomilikiwa na kuzalisha Megawatt 80 za umeme na kugawanywa katika nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.Kutokana na uzalishaji huu kila nchi hunufaika kwa kupata Megawatt 26.6 za umeme.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya uzalishaji nishati ya kanda unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Nchi husika zilianza kujenga mradi huo mwaka 2017 na kukamilisha mwaka 2022.
Akizungumza wakati ziara hiyo Mheshimiwa Balozi Kambanga alieleza kuwa mradi huo ni mfano wa utekelezaji wa diplomasia kwa njia nyingine hatua ambayo inaimarisha ushirikiano. Alisisitiza kuwa kutokana na ziara hiyo  Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda umeshuhudia uwekezaji mkubwa na upo tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo ili  iendelee kukua zaidi.

Ziara hii ni utekelezaji wa mkakati wa Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kutembelea Taasisi mbalimbali za kikanda na wawekezaji wa Tanzania wanaowekeza nchini humo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kutekeleza  diplomasia ya uchumi kwa vitendo.