Mheshimiwa Dkt. Habib Kambanga, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda ametembelea kiwanda cha uzalishaji wa mafuta ya kupikia, sabuni na vyombo vya plastiki cha Mount Meru Soyco Limited kilichopo Kayonza, Rwanda. Lengo la ziara hiyo ni kujionea shughuli za uzalishaji za kiwanda hicho ambacho chimbuko lake ni Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi ya Tanzania kwa vitendo.
Mara baada ya kuwasili katika kiwanda hicho, Mheshimiwa Balozi Kambanga alizungumza na uongozi wa kiwanda hicho pamoja na watumishi ambapo alieleza kuwa Ubalozi umepanga kuzitembelea baadhi ya taasisi za Tanzania zinazowekeza nchini Rwanda kwa kuwa unatambua mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi katika kukuza diplomasia ya uchumi.
Halikadhalika, ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya ubalozi na taasisi husika ili kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu utendaji kazi kwa lengo la kusaidia inapohitajika na mwisho alipongeza kampuni ya Mount Meru Soyco Limited kwa kuwekeza katika teknolojia endelevu nchini Rwanda.
Kwa upande wake, Bw. Manish Jain, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo alieleza kuwa Tanzania ni mshirika wa kimkakati katika ukuaji wa kiuchumi wa kanda, usalama wa chakula na maendeleo ya viwanda. Alibainisha kuwa, hatma ya Afrika Mashariki inategemea zaidi uimarishaji wa ushirikiano na kwamba Tanzania na Rwanda zina fursa kubwa na kushirikiana katika kilimo, viwanda, shoroba za kibiashara, usafirishaji, nishati na uwekezaji.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo ipo tayari kuchangia katika katika maeneo hayo kwa kukuza ushirikiano kibiashara na kuongeza thamani na mwisho alishukuru ubalozi kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.