Hatimaye historia mpya imeandikwa nchini Rwanda, baada ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), kuzindua mauzo ya gazeti la HabariLeo Toleo la Afrika Mashariki, uzinduzi uliokwenda sambamba na kongamano la kukuza lugha ya Kiswahili.
Uzinduzi huo wa aina yake na uliovuta hisia za wakazi wengi wa Jiji la Kigali nchini Rwanda ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ali Iddi Siwa. Pia hafla na kongamano hilo liliwajumuisha wageni zaidi ya 200, wakiwemo wataalamu wa Kiswahili, vyama vya urafiki baina ya Tanzania na Rwanda, wawakilishi na wamiliki wa kampuni zinazofanya biashara baina ya nchi hizo mbili.
Gazeti la HabariLeo Afrika Mashariki linalotoka mara moja kwa wiki linauzwa sambamba na toleo maalumu la Afrika Mashariki la gazeti dada la Daily News. Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Siwa aliwataka washiriki wa kongamano hilo hususani vijana kuwa mabalozi wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Alisema Kiswahili ni lugha tamu yenye historia ndefu sana ambayo pia inahusiana na ustaarabu wa maeneo kilipofikia na kwamba kukitumia vizuri kunaweza kuwa chachu ya maendeleo na mshikamano baina ya wanaokitumia lakini pia kurahisisha biashara na muingiliano. Naye Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alisema TSN ina nia ya dhati na imejipanga katika kusaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili.
Alisema gazeti lake la HabariLeo Afrika Mashariki litatumika kama nyenzo muhimu ya kufanikisha azma hiyo. “Gazeti hili litakuwa ni zana ya kujifunzia au mwalimu, wakati huo huo litaendelea kuwapatia wananchi wa Rwanda habari motomoto pamoja na burudani. Ni gazeti linalofaa kusomwa na familia nzima. “Katika kufanikisha hilo tutatumia pia utaalamu wa waandishi mahiri waliopo hapa nchini Rwanda,” alisema Dk Yonazi.
Kuhusu HabariLeo Afrika Mashariki HabariLeo Afrika Mashariki, limepania kuwa daraja la kukivusha Kiswahili kuelekea kuwa lugha rasmi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Ndilo gazeti la kwanza la Kiswahili linalochapishwa na kuuzwa katika nchi sita wanachama wa EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Ni kutokana na dhamira hiyo ndiyo maana Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki na TSN wameafikiana kuandaa makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha kufanya kazi kwa pamoja katika kukuza lugha ya Kiswahili. Ushirikiano huo utawezesha kuwa mipango mbalimbali itakayo wezesha nchi zote za Afrika Mashariki kufaidi ubora na matunda ya lugha ya Kiswahili.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Balozi Ali Idi Siwa akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi rasmi mauzo ya magazeti ya TSN nchini Rwanda. Uzinduzi huo umefanyika sambamba na Kongamano la Kiswahili lililodhaminiwa na TSN. Kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 200
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk. Jimmy Yonaz akizungumza.

